PANGANI MASHARAKI YAPIGA MARUFUKU KUPOKEA WAGENI BILA YA KUTOA TAARIFA
Wananchi katika kijiji cha Pangani Mashariki
Wilayani Pangani, wameonywa kuendelea kupokea wageni bila kuwatolea taarifa zao
kwa uongozi wa kijiji, na kwamba yeyote atakayebainika kufanya hivyo atachukuliwa hatua kali za kisheria
Akizungumza na Pangani fm Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Funguni kata ya Pangani Mashariki wilayani humo Bwana Salimu Hatibu Kiraba,
amesema kuwa wananchi katika kata hiyo wamekuwa na tabia ya kupokea wageni
kienyeji kiasi cha kusababisha maafa katika jamii, hivyo pindi msako
utakapofanyika mwenyeji na mgeni wake wote watakamatwa.
Bwana Kiraba ameongeza kuwa wananchi kutoa taarifa
kwa uongozi pindi wanapopata wageni sio ombi, bali ni agizo lililopo kisheria
hivyo amewataka waache mazoea kwani ni lazima utaratibu huo ufuatwe.
‘’Tuna tabia ya kuwapokea watu kutoka maeneo mbali
mbali wakiingia katika majumba yetu kama vile wanafamilia tunawaomba kwamba
taarifa zipatikane kwenye viongozi na
wenyeviti wa vitongoji kwa sababu unapompokea mtu kinyume na utaratibu atakuja kukamatwa kwa sababu serikali haimtambua’’ amesema Kiraba.
Aidha Bwana Kiraba amesema utaratibu huo hauangalii ndugu, jamaa wala rafiki, na taarifa zinatakiwa zitolewe hata kwa mgeni
anayelala usiku mmoja ili kuepusha usumbufu iwapo madhara yatatokea.
‘’sio wiki hata kama kaja na kalala asubuhi akafanya
safari unatakiwa kumtolea taarifa kwa sababu ni binadamu awe ndugu awe nani, binadamu anatembea na
umauti, hata kama ni baba yako unatakiwa umtolee taaarifa, akifariki nyumbani
kwako tutakushughulisha wewe’’. Amesema Kiraba.
Bwana Salimu Kiraba amesema jambo hilo mara kwa mara
wamekuwa wakilikemea lakini jamii imekuwa ikipuuza matamko kama hayo pindi wanapoyatoa,
hivyo kwasasa kumekuwa na matukio mbalimbali ikiwemo wizi uliovuka mipaka.
‘’hii hali tunaizungumzia sana lakini watu wanapuuza
na sasa hivi kuna wizi wa reja reja na hata kama tunasema huu wizi ni wa
kawaida lakini chanzo wanaotuathiri ni
wageni wanaoshirikiana na vijana wetu na kama kukatokea mgeni kaiba ni lazima
kumkamata kama ameripotiwa.’’ Amemalizia Kiraba.
Hatua hii, ni sehemu ya jitihada za kudumisha hali
ya ulinzi na usalama Wilayani Pangani, hasa kuhakikisha wageni wote
wanatambulika kila wanapofika ili wasivunje sheria za nchi.
No comments