PANGANI FM YAACHA ALAMA SIKU YA REDIO DUNIANI
(Pichani ni mkurugenzi wa shirika la UZIKWASA Bwana Novatus Urassa aliyevaa shati la rangi nyeupe na nyeusi, akifuatilia jambo wakati wa maadhimisho ya siku ya redio duniani yaliyofanyika katika hoteli ya Tanga Beach Resort)
Shirika la UZIKWASA kupitia kituo chake cha redio Pangani Fm kimeungana na wadau wengine katika kuadhimisha siku ya redio duniani, ambapo kitaifa mwaka huu imefanyika mkoani Tanga katika hoteli ya Tanga Beach Resort.
Maadhimisho hayo ambayo yamejumuisha waandishi wa habari wa vyombo vya habari vya jamii kutoka Tanzania Bara na Visiwani na Wadau wengine wa habari, yameratibiwa na shirika la UNESCO kwa kushirikiana na Mtandao wa Redio Jamii Tanzania (TADIO), huku mgeni rasmi akiwa ni naibu waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mheshimiwa Julianza Shonza.
(Pichani aliyevaa miwani ni Bi Maajabu Ally akifatilia kwa makini maadhimisho ya siku ya redio duniani)
Katika maadhimisho hayo Pangani Fm ilipata nafasi ya kuonyesha na kugawa vipeperushi vyake vinavyoonyesha shughuli zinazofanywa na shirika la UZIKWASA, ikiwa ni pamoja na kalenda za mwaka 2019, majarida ya filamu ya Aisha, filamu ya Aisha iliyokuwa kwenye mfumo wa DVD pamoja na filamu ya Chukua Pipi ambazo zote zimetengenezwa na shirika hilo.
Mbali na ugawaji huo, pia Pangani Fm imepata nafasi ya kueleza namna ya utengenezaji na urushaji wa vipindi vyake vinavyogusa jamii na kubadilisha mtazamo hasi, sambamba na kuleta uwajibikaji kwa viongozi kutokana na mafunzo ya uongozi wa mguso yanayotolewa na shirika la UZIKWASA.
Maajabu Ally Madiwa ambaye amekuwa akifanya kipindi cha Sauti Ya Mwanamke kinachorushwa na Pangani Fm amewaeleza waandishi wa habari na wadau wengine waliohudhuria siku hiyo ya redio duniani, namna redio ilivyosaidia kuokoa maisha ya akina mama wajawazito waliokuwa wakijifungulia eneo la Bweni kwa kukosa kivuko cha dharura wakati wa Usiku, ambapo baada ya kipindi kuruka serikali ilifanya jitihada za kuweka kivuko cha dharura.
Pia Bi Maajabu aliweka bayana kuhusu mada nyengine ambayo pia iliibua hisia kwa wadau wa habari, juu ya hofu ya talaka inavyopelekea baadhi ya wanawake waliopo kwenye ndoa kufanyiwa vitendo vya ukatili, ikiwa ni pamoja na kuombwa unyumba kinyume na maumbile.
Mada ambayo baada ya kuruka hewani, ikaibua wanawake wengi waliokuwa wanaogopa kusema hali halisi wanayokutana nayo, kiasi cha kufanya maamuzi ya aidha aachane na ndoa ama amueleze ukweli mumewe kuwa kitendo anachokifanya dhidi yake ni ukatili.
Mbali na Maajabu, washiriki wengine kutoka shirika la UZIKWASA ambao walihudhuria maadhimisho hayo ni Mkurugenzi wa shirika hilo ndugu Novatus Urassa, Meneja wa kituo cha redio Pangani Fm Bi Maimuna Msangi pamoja na Mhariri wa kituo hicho Ndugu Mohammed Hammie.
(Pichani ni meneja wa kituo cha redio Bi Maimuna Msangi akifuatilia maadhimisho hayo)
Kauli Mbiu ya siku ya Redio mwaka 2019 ni majadiliano, uvumilivu na amani, ikiwa na maana ya kutambua nguvu ya radio katika kushawishi majadiliano chanya, kuvumiliana na kuendeleza amani ulimwenguni.
No comments