UZIKWASA YAONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA UKATILI PANGANI


Upotevu wa ushahidi, rushwa, udugu na ushirikiano hafifu wa wanajamii vimetajwa kuwa changamoto ya uendeshaji wa kesi za matukuo ya ukatili wilayani Pangani.

Hayo yamezungumzwa na wadau wa kupinga vitendo vya ukatili wilayani humo (Kikosi Kazi) katika kikao cha pamoja kilichofanyika ukumbi wa YMCA uliopo Mkoma wilayani Pangani chenye lengo la kuweka mbinu za kupinga matukio ya ukatili Wilayani humo.



Wakiwasilisha changamoto wanazokutana nazo katika uendeshaji wa kesi za matukio ya ukatili baadhi ya wadau walioshiriki kikao hicho wamesema kuwa kwa kukosa uadilifu baadhi ya waendesha mashtaka wamekuwa wakihairisha kesi kutokana na kupewa rushwa, sambamba na mashuhuda kuuminya ushahidi hasa ndani ya familia.

‘’Kwa mfano ukikuta mwendesha mashtaka amekosa uaminifu anavutwa pembeni na kupewa kitu kidogo kwa kukosa uadilifu  anachukua na kuandika taarifa za uongo na wakati mwingine utasikia anamwambia hakimu” amesema Mjumbe.

Pamoja na changamoto hizo wadau hao wameelezea mafanikio yao ikiwemo kuwepo kwa mfumo wa uripotiwaji wa matukio ya ukatili ulioundwa na shirika la UZIKWASA ambao umepelekea watoto kuongea bila woga ikiwemo ushirikiano uliokuwepo kati ya idara husika na madaktari.

‘’Lakini mfumo mwingine tutawaangalia sana wenzetu wa shirika la UZIKWASA na nawapongeza sana wamekuwa mstari wa mbele wa kuweka jitihada na mipango mingi katika kukabiliana na hili jambo na kuweka mfumo flani wa kuripoti matukio kwa kupita katika mashule na wameweka mawakala na mabalozi’’ amsema mmoja wa wajumbe.


Kwa upande wa afisa TAKUKURU wilayani pangani Bwana Joseph Paul ametoa wito kwa wadau hao kujikita zaidi katika utekelezaji kwa kina ili kuhakikisha matukio ya ukatili yanapungua.

‘’Kwa upande wangu nitoe tu wito kwamba tuongeze kasi ya utekelezaji wa jambo hili na huu mpango ndo iwe dira yetu, tutoke kule kwenye mkwamo tuingie kwenye utekelezaji kwa sababu haya mambo huwa yanatokea sana’’amesema Bwana Paul



Akihitimisha mazungumzo hayo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Bwana Isaya Mbenje amesema kuwa wadau wana kazi kubwa sana ya kupambana na matukio ya ukatili ili kubadilisha mwelekeo wa watu wanaoishi nao.

‘’Kwa hiyo tuna kazi kubwa sana ya kufanya na kuhakikisha kwamba tunapambana na vitendo vya ukatili, zaidi sana kubadilisha mwelekeo wa watu tunaoishi nao, nimejaribu kujifunza hapa kwa haraka haraka naona kwamba hapa ni tofauti na sehemu nyingine, mimi huko nilipokuwa tulikuwa na program za kupinga ukatili, lakini ukiangalia ukatili unatokana na nini kule kwa wenzangu huwa wanatafuta utajiri yaani kuna imani kwamba ukimbaka mtoto mdogo unapata utajiri, ukimuua sijui flani unapata mali yaani kunakuwa na mwanzo, lakini kwa mazungumzo haya ya leo sijaona kama mtu anafanya ukatili ili apate utajiri’’ amesema mkurugenzi



Kikosi kazi cha kupinga matukio ya ukatili wilayani pangani kinajumuisha wadau mbali mbali ikiwemo idara ya elimu, afya, maendeleo ya jamii, jeshi la pilisi na mahakama, takukuru, maafisa tarafa wilaya huku kikiongozwa na mkuu wa wilaya hiyo Bi Zainabu Abdallah Issa.

No comments

Powered by Blogger.