WAITARA ATEMA CHECHE PANGANI
Naibu Waziri ofisi ya Rais TAMISEMI mheshimiwa Mwita
Mwikwabe Waitara ameagiza kusimamishwa kazi afisa mipango wa halmashauri ya
wilaya ya PANGANI Bwana Waziri Mwakibolwa kutokana na kusua sua kwa utendaji
wake.
Naibu waziri Mwita amesema Hayo kupitia ziara ya
siku moja aliyoifanya wilayani pangani wakati akizungumza na watumishi wa
halmashauri hiyo yenye lengo la kuangalia tathimini ya utendaji kazi baada ya
kutembelea baadhi ya shule za serikali.
Amesema Kusimamishwa kazi kwa Bwana Mwakibolwa kumetokana
na malalamiko mbali mbali ikiwemo utendaji kazi mbovu, ukosefu wa nidhamu, ulevi
huku akiwataka viongozi wa halmashauri kutoa taarifa kama wanaupungufu wa
watendaji.
‘’Kwa
hiyo huyu asimamishwe kazi mara moja kutokana na malalamiko dhidi yake na sio
leo ana mengine ya utovu wa nidhamu na watu wameshaleta taarifa nyingi tofauti
na hizo za mkuu wa mkoa, natambua kuna taarifa nyingi kule ofisini kwamba hapa
kuna shida ya afisa mipango, kama kuna shida ya upungufu wa watumishi hapa ije
ajenda maalumu ya kiofisi.’’
Mheshimiwa Waitara pia amekemea tabia za viongozi
kuwarudisha kazini watumishi waliosimamishwa kazi bila ya kufuata taratibu za
kisheria huku akimtaka kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Bwana Daudi
Mlahagwa kuandika barua ya kuomba radhi kutokana na kukiuka maamuzi ya ngazi za
juu na kumrudisha kazini Bwana Mwakibolwa ambaye alisimamishwa kazi na mkuu wa
mkoa wa tanga Bwana Martin Shigela.
‘’Ili mtu arudushwe kazini ni lazima timu
ifanyie kazi, kwamba hizi taarifa ambazo tunazo kama ni chuki, ni husda vyote
vinatakiwa vijulikane, kwa hiyo hii habari ya kuwatumia madiwani kuja
kujiridhisha watu ambao wanalalamikiwa na kufanya mkuu wa mkoa aje aonekane
kuwa hamna kitu, kwa sababu anatoa maagizo alafu watu wanakuja kuyapinga, na
huyu kaimu mkurugenzi anatakiwa kuandika barua ya kuomba radhi kwa kukiuka
maagizo ya ngazi ya juu”
Awali mkuu wa mkoa wa tanga Bwana Martin Shigela alimuagiza
aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Pangani Bwana Daudi Mlahagwa kumsimamisha
kazi afisa mipango wa halmashauri ya hiyo Bwana Waziri Mwakibolwa kutokana na
malalamiko yaliyotolewa kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichojadili kutotumika
kwa fedha za mfuko wa jimbo hadi kuvuka mwaka bila ya matumizi hali ya kuwa
wananchi wanauitaji nazo.
No comments