WANANCHI PANGANI WATAKIWA KUTOA USHIRIKIANO KWENYE VYOMBO VYA SHERIA
Wananchi wametakiwa kutoa ushirikiano kwenye vyombo vya
sheria hasa katika suala la kutoa ushahidi, ili kuhakikisha mashauri
yanayofikishwa Mahakamani yanamalizika kwa wakati.
Wito huo umetolewa leo na Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo
Pangani Mjini Bwana Jordan Abraham kwenye Mazungumzo Maalum na kituo hiki,
ambapo amesema kuwa ni muhimu kuwekeza nguvu nyingi katika kuhakikisha mashauri
yanayofika kwenye ngazi ya Mahakama yanamalizika kwa wakati, kwani licha ya
kupatikana kwa haki, kuna okoa muda na fursa ya kufanya shughuli za kujiingizia
kipato.
“Sasa
jambo linapokuwa limeisha kwa wakati tafsiri yake ni kwamba huyu mtu anapata
fursa ya kuweza kupanga kufanya mambo yake mengine, kwa hiyo kuanzia mwananchi
wa kawaida niwaombe tushirikiane na wadau hawa wenye kupewa mamlaka ya kufanya
uchunguzi wa mashauri mbalimbali, lakini pia vyombo vyetu vya uchunguzi navyo
vifanye kazi zao kwa weledi kwa kuzingatia sheria na taratibu na ukomo wa muda
uliowekwa kisheria ili kuzipa urahisi mahakama zetu ziweze kufanya hayo maamuzi
kwa wakati na hatimaye haki iweze kuonekana sio tu kutendekea bali pia ionekane
imetendeka na imetendeka kwa wakati”alisema Hakimu JordanAbraham
Bwana Jordan ameongeza kuwa tukiwa ndani ya wiki ya Sheria
itakayofikia tamati tarehe 6 mwezi huu wa pili, pia maadhimisho hayo
yataambatana na utoaji wa elimu kuhusu masuala mtambuka ya kisheria, kulingana
na kauli mbiu ya mwaka husika, ambapo mwaka huu wa 2019 maadhimisho hayo
yamebebwa na kauli mbiu isemayo “UTOAJI
WA HAKI KWA WAKATI,,,WAJIBU WA MAHAKAMA NA WADAU”.
Hata hivyo amezungumzia namna walivyojipanga kuadhimisha
wiki hiyo ya Sheria kwa kutembelea maeneo mbalimbali kutoa elimu, kuhusu namna
njema ya wananchi kuzifikia mahakama kwa urahisi na kupata haki zao.
“Tumejipanga vyema kama ilivyo ada yetu kwa kila mwaka, na kipaumbele
chetu kikubwa ni kutoa elimu ya sheria. Jana tumekwenda kwenye shule mbalimbali
za msingi na secondary ambako tumepata fursa ya kukutana na hadhara ya
wanafunzi na kuweza kuwaelimisha kuhusiana na mambo kadha wa kadha ya kisheria”
Alisema Hakimu Jordan Abraham
Maadhimisho ya Wiki ya Sheria, mbali na kuadhimishwa kwa
kutoa elimu mbalimbali kuhusu masuala ya kisheria yanayotatiza, pia inaashiria
kuanza kwa Mwaka mpya wa Mahakama.
No comments