HALMASHAURI YA PANGANI YADHAMIRIA KUMALIZA UJENZI WA KITUO CHA AFYA MWERA KWA WAKATI




Halmashauri ya Wilaya ya Pangani imeanza mchakato katika Mradi wa kuboresha kituo cha Afya kilichopo eneo la  Mwera kwenye utoaji wa huduma, mradi ambao unatakiwa kukamilika ndani ya siku tisini tangu ulipoingiziwa fedha.

Wakiameambatana kwa Pamoja katika mazungumzo maalum na kituo cha Pangani Fm, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Pangani Daktari Juma Mfanga na Msimamizi wa Miradi mbalimbali ya kimaendeleo wilayani humo ambaye pia ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bwana Sabas Damian Chambasi, wamesema kuwa kiasi cha fedha Milioni 400 ambacho wamekipokea kutoka serikali kuu, zinapaswa kutumika ipasavyo kwa ushirikiano wa pamoja, ili kuhakikisha ndani ya miezi mitatu mradi huo unakamilika kama inavyotakiwa.

Kwa upande wake Bwana Sabas amehimiza ushirikiano wa pamoja katika hatua za awali mpaka kukamilika kwa mradi, ndio msingi wa kukamilika kwa wakati.

“Mnamo tarehe Desemba 27, 2017 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilituletea fedha kiasi cha shilingi milioni Mia Nne, hizi fedha zimekuja zikiwa na muongozo lakini huo muongozo unatuhitaji sana tushirikishe wananchi katika kuhakikisha kwamba hizo fedha zinatumika”. Amesema Bwana Sabas Chambasi na kuongeza kuwa……



“Tunataka kwenda kuboresha kituo cha afya Mwera inatakiwa ushirikiano kati ya serikali, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo, siku ambazo tumepewa kwa ajili ya kukamilisha mradi kuanza na kukamilisha mradi ni siku tisini tu maana yake ni nini miezi mitatu tu, ili kukamilisha mradi huu inatakiwa wote tushirikiane katika kununua, kuhakiki, tuanze kwa pamoja na tumalize kwa pamoja tukiwa na kasi mpaka tunamaliza”. Amesema Mkurugenzi huyo 



Kwa Upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani Dokta Juma Mfanga, mbali na kusema mradi huo unakwenda sambamba na kuongeza wataalam katika kituo hicho, pia amesema ziko fedha nyingine zilizotengwa kwaajili ya kununulia vifaa tiba.

“Kama kituo kikikamilika kesho tungeendelea kufanya upasuaji mana sisi katika hospitali ya halmashauri tuko saba pamoja na kwamba ikama ya madaktari inasema hospitali ya wilaya iwe na madaktari nane wenye digree ya miaka mitano, lakini population ya huku ni ndogo kuliko wilaya nyingine, ila shuleni wako wawili wanasoma wakirudi wanakuwa tisa.  Kwa hiyo kumtoa mtaalam kumpeleka pale sio tatizo na juzi tumepata wengi tu wa ajira mpya na wengi tumewapeleka pale makusudi kwa sababu baada ya miezi mitatu kituo kitaanza kufanya kazi”. Amesema Bwana Mfanga na kuongeza kuwa…..

Daktari Mfanga ameongeza kuwa katika suala la Afya hakuna siasa wala dini, hivyo uboreshaji wa kituo cha Afya Mwera ni suala linalopaswa kutekelezwa na watu wote bila kujali itikadi zao, akisema maendeleo ni suala linaloletwa kwa pamoja na si kwa kujitenga.

“Ni vizuri watu wakaelewa kitu kimoja katika suala la afya hakuna siasa ukishakuwa unaumwa hautibiwi na hospitali ya chama fulani au ya dini fulani, sisi kazi yetu ni kusimamia kazi za serikali na tuko hapa kwa ajili ya serikali, kwa hiyo katika suala la kituo cha afya Mwera linatakiwa kutekelezwa na watu wa dini zote pia vyama vyote”. Amesema Daktari Juma 

Tarehe 27 mwezi wa 12 mwaka jana wa 2017, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliingizia halmashauri ya wilaya ya Pangani kiasi cha shilingi milioni 400 kwa ajili ya uboreshaji wahuduma za afya katika kituo cha Mwera, huku halmashauri hiyo ikipewa siku tisini yaani miezi mitatu kuhakikisha mradi huo unakamilika kama inavyopaswa.

No comments

Powered by Blogger.