MKANDARASI ATAKIWA KUKAMILISHA UJENZI WA JENGO LA HALMASHAURI YA PANGANI HARAKA



Mkandarasi anayeshughulikia ujenzi wa jengo jipya la halmashauri ya wilaya ya Pangani ametakiwa kuongeza kasi ya ujenzi wa jengo hilo ili  kulikamilisha kwa wakati na kuweza kutumika.

Maagizo hayo yametolewa leo na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya rais Tawala za Mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa JOSEPHAT SINKAMBA KANDEGE wakati wa ziara yake wilayani  humo, ambapo amesema  ujenzi wa jengo hilo ulikuwa umesuasua kwa muda mrefu na hivyo amemtaka mkandarasi huyo kuongeza kasi ya ujenzi ili kukamilisha ofisi hizo.

’jengo hili kama nilivyowaambia kuwa limeanza kujengwa kwa muda mrefu na taarifa nilizokuwa nazo ni kuwa tayari halmashauri imeshapokea fedha kiasi cha shilingi milioni mia saba lakini matumizi yake yalikuwa yanaenda kwa kusua sua sana  kiasi cha mkandarasi aondoke saiti lakini leo nimefika pale na nimemkuta, kikubwa ninachomwambia ahakikishe kuwa anafanya haraka ili jengo la ofisi ziweze kukamilika.’’ Amesema Mh. Kandege.



Katika kuendelea na ziara hiyo mheshimiwa Naibu Waziri JOSEPHAT KANDEGE ametembelea kituo cha Afya Kata ya Mwera ili kuona maendeleo ya kituo hicho katika kutoa huduma ambapo mara baada ya kuona jengo la upasuaji amesema kuwa halijajengwa kama  ilivyotakiwa na kuagiza jengo hilo likamilishwe katika kiwango kizuri.

’kwa sababu jengo limeshajengwa na halikukamilika na ukitizama jengo hili limejengwa na ramani iliyotolewa na ofisi ya Tamisemi kuna tofauti kidogo lakini tofauti hiyo inaweza ikavumilika na kwa sababu pesa imeshatumika kiasi cha milioni ishirini na tano (25), hatuwezi kusema pesa hii ambayo imetumika ipotee hivi hivi kwa hiyo katika hizo pesa walizopata shilingi milioni mia nne ni pamoja na kukamilisha hiyo theater tarajiwa lakini wakamlishe kwa kiwango kizuri’’ Amesema Mh. Kandege.



Aidha Mheshimiwa Naibu Waziri amewataka watumishi wote wa Serilaki kupitia Halmashauri ya wilaya ya Pangani kuhakikisha wanawajibika ipasavyo katika kuwatumikia wananchi ili kuleta maendeleo kwa wilaya na Taifa zima kwa ujumla.

Lengo la ziara hiyo ni kukagua shughuli mbalimbali za kimaendeleo pia na  kuona namna ujenzi wa kituo cha Afya Mwera, na kuona maendeleo ya  jengo la halmashauri ambalo ujenzi wake unaendelea.

No comments

Powered by Blogger.