MADAKTARI PANGANI WAZUNGUMZIA HATARI YA UGONJWA WA U.T.I



Ugonjwa wa njia ya haja ndogo kwa maana ya U.T.I Wilayani Pangani unatajwa kuwa miongoni mwa magonjwa sugu kumi yanayowatesa watu wengi kwenye jamii, ikifuatiwa na Magonjwa ya njia za hewa.

Akizungumza katika kipindi cha ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki, Mtaalamu wa masuala ya kinamama katika hospitali ya wilaya ya Pangani Daktari KOMBO MUHINA amesema kuwa miongoni mwa Magonjwa hayo yanayosumbua Wilayani humo Ugonjwa wa U.T.I unashika nafasi ya Pili ukiongozwa na magonjwa ya Njia za hewa.

“Katika magonjwa kumi yanayosumbua Pangani, ugonjwa wa njia za Mkojo unashika nafasi ya pili katika hospitali yetu na katika wilaya yetu ya Pangani, ndio maana tumeona ni vizuri kulizungumza ili wananchi waweze kuelewa. Linaloongoza ni magongwa ya njia za hewa, hili ndio tatizo kubwa la kwanza likifuatiwa na hili la njia ya mkojo” Amesema Daktari Kombo Muhin.



Wakizungumzia ukubwa wa tatizo la ugonjwa wa U.T.I Madaktari kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Dokta Pasco Madukwa na mwenzake Ruben Nyasusa, wamesema ugonjwa huo umeenea kwa kiasi kikubwa hapa nchini na unaendelea kuwatesa watanzania walio wengi, huku wakitanabaisha sababu za ugonjwa huo.

“Kimsingi tatizo kubwa sana, sehemu nyingi ambazo tumezunguka hapa Tanzania utalikuta katika hospitali linakuwa ni tatizo namba moja au namba mbili, kwa sababu gani, watu hawa tunawatibu lakini wakitoka wanarudi katika yaleyale mazingira ambayo ni hatarishi, lakini kingine kuongezea hapa ambalo pia ni onyo vilevile kwa wakazi wa Pangani na sehemu zingine ni kwamba inabidi usitumie dawa yoyote pasipo kuandikiwa na daktari” wamesema Madaktari hao kutoka Muhimbili na kuongeza kuwa…….

“Kama mtu ugonjwa wake umefikia hatua ya mbali na akapata matibabu ambayo si sahihi, ugonjwa huo utajirudia na kujirudia.


Ili kufanikiwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo madaktari hao wameshauri wananchi kufika mapema katika vituo vya kutolea huduma za Afya, pamoja na kushauri jamii kujali usafi kuanzia wa mwili na mazingira wanayoishi.

 “Baada ya matibabu mtu anatakiwa azingatie kutumia maji mengi, usafi wake wa mwili lakini pia usafi na watu wale wanaomzunguka ili ugonjwa usiwe kwake tatizo na kwa jamii pia ambayo inakuwa inamzunguka, wakifanya hayo tatizo hili litashuka chini” Wakiongea kwa msisitizo wataalamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Imeelezwa kuwa ugonjwa wa U.T.I unaweza kumpata mtu yeyote bila kujali jinsi yake na umri, ijapokuwa kutokana na sababu za kibaiologia na kinga ya mwili kushuka au kuwa ndogo yapo makundi ambayo huathirika zaidi ikiwemo watoto, wazee na wanawake.
 
Kadhalika Dalili za ugonjwa huo zinaweza kuwa kusikia maumivu wakati wa kujisaidia haja ndogo, homa na maumivu katika viungo vya mkojo, kuhisi kuhitaji kujisaidia haja ndogo mara kwa mara na pia haja ndogo kuwa na hali ya kuunguza wakati wa kujisaidia.

No comments

Powered by Blogger.