WANAFUNZI 308 WA KIDATO CHA KWANZA WARIPOTI PANGANI



Takribani wanafunzi 308 kati ya 754 waliotakiwa  kuijiunga  na  kidato cha kwanza kwa mwaka  2018  tayari wameripoti katika shule  mbali mbali wilayani Pangani ili kuanza masomo yao ya Sekondari.

Akizungumza  na Pangani Fm ofisini  kwake Kaimu Afisa Elimu  Sekondari  wilayani humo Bwana ALI MWIN’CHAGA mbali  na kueleza hali ya wanafunzi kuripoti kujiunga na kidato cha kwanza, lakini pia amesema kuwa wamepata msaada kutoka  UK AID ambao wametoa  vitabu mahususi vitakavyowasidia  wanafunzi hao kumudu  masomo  ya sekondari kwa mwaka huu.

 ‘’Sasa katika kufungua shule mpaka sasa hivi wameripoti wanafunzi 308 kwa kuwa wanafunzi hawa walikuwa wanajifunza masomo yote kwa lugha ya Kiswahili na sasa hivi wanakwenda elimu ya sekondari na watajifunza masomo yao kwa lugha ya Kingereza na tumepata msaada wa british council na UK AID hawa wametuletea vitabu mahususi kwa ajili ya kuwafundisha hawa watoto wanaotoka elimu ya msingi ili kupata msingi wa kuanzia masomo ya sekondari.’’ Amesema Mwin’chaga.



Aidha Bwana MWIN’CHAGA ameongeza kuwa  kutokana  na vitabu  hivyo walivyopokea kuwa ni vipya wamelazimika kutafuta  mtaalamu ambaye  atawajengea  uwezo baadhi  ya walimu katika shule za sekondari ambao watafundisha wanafunzi hao wanaojiunga  na kidato  cha kwanza.

‘’Kwa sababu vitabu ni vipya tulivyoletewa tumefanya  yafuatayo, kwanza vitabu ni vipya tunajuwa wazi kuwa itakuwa ni mtihani kwa baadhi ya walimu ilibidi sasa tutafute mtaalamu wa kuendesha semina na mtaalamu huyu aweze kuendesha semina kwa kila shule ili kuwajengea uwezo walimu watakao wafundisha wanafunzi ambao tunawapokea wa kidato cha kwanza’’ Amesema Mwin’chaga.

Sambamba  na hilo  Bwana MWIN’CHAGA amesema kuwa ni matarajio kuwa  kiwango  cha ufaulu  kwa  mwaka 2018 kitapanda  na kuzitaka shule  binafsi wilayani humo kujifunza  kutoka  kwa shule nyingine zinazofanya vizuri  hapa  nchini.

No comments

Powered by Blogger.