WAKAZI WA PANGANI MASHARIKI WATAKIWA KUFUATA VITAMBULISHO VYAO VYA TAIFA OFISI YA KATA



Wananchi katika kata ya Pangani Mashariki hususani wote walioandikishwa vitambulisho vya ukazi/taifa kisha majina yao kurudi bila vitambilisho katika zoezi lililopita, wametakiwa kufika kwenye ofisi yao ya kata kwa ajili ya kupatiwa vitambulisho vyao.

Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya mwemyekiti wa kijiji cha Pangani Mashariki Mhe. Haji Nundu, mwenyekiti wa kitongoji cha Funguni Bwana Salimu Hatibu Kiraba amesema kuwa wote wanaoguswa katika hili ni muhimu kufika ofisi ya kata ili kupatiwa vitambulisho vyao.

Pamoja na kuelezea umuhimu wa kitambulisho cha ukazi amesema zoezi la utoaji wa vitambulisho hivyo katika kata yake, litafanyika kila siku ya Jumaatatu hadi Ijumaa kuanza majira ya saa mbili asubuhi hadi saa tisa Alasiri.
‘’ Kwa niaba ya mwenyekiti wa kijiji cha pangani mashariki taarifa hii ni wale ambao waliandikisha vitambulisho vya ukazi na bahati mbaya majina yao yamerejeshwa bila vitambulisho vyao kuambatana nayo mnatangaziwa kwamba vitambulisho hivyo vimeshapatikana vipo ofisi ya kata mtendaji kata wa pangani mashariki kwa siku ya jumatatu ukienda utavikuta kwa sababu kitambulisho ni muhimu na ndicho kitakachokufanya wewe utambulike kama mtanzania’’ amesema Kiraba.



Aidha Bwana Kiraba ametumia nafasi hiyo pia kuwataka watu ambao hadi sasa ndani ya kitongoji chake wamepoteza vitambulisho vyao vya uraia, nao kufika katika ofisi za kata na kutoa taarifa ili kupatiwa mwongozo ambao utawawezesha kushiriki hata kupiga kura.

‘’wale ambao wapo kwenye kata yangu au kijiji changu cha pangani mashariki ukiona umepoteza kitambulisho chako cha kupiga kura nenda ofisi ya mtendaji wa kijiji ambapo utatoa taarifa zako utapata mwongozo ambao utakusaidi kupata kitambulisho chako au hata kama uchaguzi umekaribia utapata barua ambayo itakufanya uweze kutambulika’’ ameongezea Kiraba.

Kadhalika amewataka wote ambao wakati zoezi la uandikishaji wa vitambulisho vya ukazi hawakuwepo ndani ya wilaya, wawasilishe taarifa zao ili kusajiliwa, kwa kuwa zoezi hilo hufanyika kila mwaka.
‘’ kuna wengine walikuwa hawapo katika maeneo husika vitambulisho vinaandikishwa walikuwa nje ya wilaya na wamerudi, basi waripoti kwa mwenyekiti wao wa kijiji ili wakatoe taarifa zako upewe barua ya ukazi itakayokusaidia kupiga kura’’ amemalizia Kiraba.

Lengo la serikali ni kuhakikisha inafanikiwa kuwasajili na kuwatambua wananchi wake wote, na zoezi hilo humgusa kila mwananchi aliyefikisha umri wa miaka 18 na kuendelea.

No comments

Powered by Blogger.