NGUVU YA PAMOJA NDIO CHACHU YA KUTOKOMEZA UKATILI WA KIJINSIA KIJIJI CHA KIMANG'A WILAYANI PANGANI



Nguvu ya Pamoja katika kutekeleza mipango ya kimaendeleo kijiji cha Kimang’a, inaelezwa kuwa ndio mwarobaini utakaokomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia kijijini hapo.

Wakizungumza mapema hii leo katika kipindi cha ASUBUHI YA LEO kinachorushwa na kituo hiki, baadhi ya wajumbe wa kamati ya kudhibiti Ukimwi Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Kimang’a wamesema kuwa siku za nyuma hawakuweza kufanikiwa kutokana na kukosekana Ushirikiano na Umoja miongoni mwao.

Aidha Bwana Daudi Bushishi ambaye ni Katibu Msaidizi kwenye Kamati hiyo, amesema kuwa siri ya kamati yao kupata mafanikio ni umoja, maelewano baina yao pamoja na kushikamana tangu wapopatiwa elimu ya uongozi wa mguso.



Naye Bi Maria Peter ambaye ni mmoja ya wajumbe katika kamati hiyo, kufuatia mkasa aliowahi kupitia wa kukatishwa masomo kutokana na vishawishi alivyokutananavyo, ametumia nafasi hiyo kuwaonya mabinti wengine ambao kwasasa wanakumbana na vishawishi hivyo kutokubali kudanganyika.

“Kwa kweli roho yangu inauma sana. Wasichana wenzangu, wanawake wenzangu na hata wanafunzi kuweni makini, mimi kama Maria maisha yangu ya pale kijijini kwetu Kimang’a watu wanayaelewa, nilivunjiwa masomo baada ya kushawishiwa na vijana na baadae kupewa ujauzito, ndoto za kielimu zikaishia hapo. Sasa nawaambia bila elimu sasa hivi sawa na bure, unachotakiwa ni kusoma hayo mambo mengine utayakuta, hao wanakulaghai tu! Wakikukuta watapuka elfu moja, elfu mbili mwisho wa siku watakuvunjia ndoto zako, nawausia kuweni makini” Amesisitiza Bi Maria.

Bi Maria amemalizia kwa kusema ili kukomesha kabisa vijana waliojikoki kukatisha ndoto za kielimu kwa watoto wakike, ushirikiano wao ndio utakuwa mwarobaini tosha kwa kuwakamata, na kuhakikisha wanaozea katika mikono ya sheria.



“Tutakapo wakamata tuwafikishe katika vyombo vya sheria, na baada ya kuwafikisha huko isiishie hapo, bali tuhakikishe wote walioshikwa baada ya kubainika kazi yao ilikuwa ni kuwaharibia maisha watoto wa kike, wanaozea katika mikono ya sheria, nadhani huu utakuwa mwarobaini hasa wa kukomesha tabia mbovu za watu hao katika kijiji chetu”Amesema Bi Maria Peter.

Kamati ya Kudhibiti Ukimwi Jinsia na Uongozi VMAC ya kijiji cha Kimang’a, imeshika nafasi ya 7 katika tamasha la kutafuta kamati bora mwaka 2017, kutoka nafasi ya 22 iliyokamata mwaka 2016, nah ii ni kutokana na kukua kiutekelezaji wa mipango mkakati.

No comments

Powered by Blogger.