UPATIKANAJI WA MAJI PANGANI MJINI WAIMARIKA BAADA YA UKARABATI WA MIUNDOMBINU



Zoezi la ukarabati wa miundombinu ya Maji wilayani Pangani hususani Pangani Mjini hatimae umekamilika, huku ikikadiriwa eneo lenye urefu wa mita 3350 likipata maji kwa uhakika.

Akizungumza na Pangani FM meneja wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Pangani Mjini Bwana Adamu Waziri Sadiki, pamoja na kuthibitisha ukamilifu wa zoezi hilo amesema kuwa kwa wateja ambao wamepitiwa na ukarabati huo na bado hawapati huduma ya maji, wafike kwenye ofisi zao zilizopo katika jengo lilokuwa ofisi ya mkuu wa wilaya zamani ili kuwasilisha matatizo yaliyopo

 ’lile zoezi letu la kuifanyia ukarabati miundombinu ya maji hasa maeneo ya pangani mjini limekamilika na limetumia takribani urefu wa mita 3350, kama kuna mwananchi hapati maji afike ofisini kwetu’’ amesema meneja wa maji.

Pia Bwana Adamu ameongeza kuwa wadaiwa sugu hawatapata huduma ya maji hadi watakapolipa madeni yao, na kwamba ili huduma hiyo ikidhi mahitaji ni lazima wateja kulipa kwa wakati.

’pia kuna watu ambao ni wateja wetu ni wadaiwa sugu, kwa hiyo watu kama hawa hatukuwaunganishia maji, tunaomba mje mlipe na ukiona bomba limepita na huja unganishiwa ujuwe ni mmoja wa wadaiwa sugu mlipe ili tuwaunganishie’’ ameongeza tena.

Ukarabati wa miundombinu mipya ya maji Pangani Mjini umehusisha ufukuaji wa mabomba chakavu na kufukia mapya, na hii ni katika mpango wa kuhakikisha huduma ya maji safi na salama unawafikia wananchi wote kwa urahisi.

No comments

Powered by Blogger.