WAKULIMA PANGANI WAIPONGEZA IDARA YA KILIMO KWA KUWAELIMISHA KUHUSU ZAO LA KOROSHO.



Idara ya kilimo wilayani Pangani imepongezwa kwa jitihada zake za kuelimisha wakulima katika zao la korosho jambo lililopeleka wakulima hao kutumia njia mbalimbali za kitaalamu ikiwemo kupulizia dawa na kulimia mikorosho yao kwa wakati.

Akizungumza na Pangani FM Mkulima mmoja wa zao hilo kutokea kijiji cha Sange aliyejitambulisha kwa jina la ALBANO PETER MWALIDO amesema kutokana na hali hiyo imewawezesha wakulima kupata mavuno mengi katika msimu huu.

‘’Kwenye elimu ya mikorosho kwa kweli serikali imejitahidi na halmashauri pia imejitahidi, imehamasisha na kuelekeza wakulima hasa kata ya mkwaja wakulima wengi wanaendana na wakati watu wengi walijitahidi kusafisha mashamba na kupulizia dawa jambo ambalo limepelekea wakulima wengi kuvuna korosho’’amesema Albano.

Mbali na mafanikio hayo Bwana Albano amesema bado wanaathiriwa na kuchelewa kwa msimu mpya wa mnada wa korosho,  hali inayopelekea baadhi ya wakulima kuuza mazao yao kwa wafanyabiashara wa maduka kwa bei ndogo.

‘’wakulima wengi wana korosho ndani wengine wana gunia tatu hadi nne lakini changamoto kubwa hawajui watamuuzia nani, na zitauzwa lini, sasa kilichokuwepo mkulima huyu analanguliwa.’’ Amesema Albano.

Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Pangani Bwana RAMADHANI ZUBERI amesema wakulima wanapaswa kupeleka mazao yao kwenye chama cha ushirika katika kijiji cha Mikocheni, ili kuwezesha kupata idadi kamili ya mazao yote ndipo waitishe mnada.

‘’Wakulima wote kila mmoja korosho zake apelike kwenye chama cha ushirika pale wakazipime zipo kiasi gani ili baadae tutakapo zikusanya tutatangaza kwenye bodi na ili kutafuta mnunuaji na huo ndo utaratibu ulio pangwa kuwa korosho haziuzwi kwa kilo moja moja’’ amesema Zuberi.

Zao la korosho ni miongoni mwa mazao ya biashara nchini Tanzania ambalo limeonekana kuwanufaisha wakulima wa zao hilo kutokana na kutumika mfumo wa mnada hususani katika mikoa ya lindi na mtwara, huku katika wilaya ya Pangani idara ya kilimo ikiendeleza jitihada zake katika kuinua thamani ya zao hilo.

No comments

Powered by Blogger.