RIPOTI YA AFRIWAG YAZINDULIWA RASMI LEO WILAYANI PANGANI



Kufuatia ripoti ya utafiti na tathmini iliyoandaliwa na taasisi ya AFRIWAG na Twaweza kuonyesha uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa chakula shuleni huku kiwango cha mahudhurio ya wanafunzi na walimu kikionekana kupita makadirio ya taifa, walimu na wadau wa elimu Wilaya ya Pangani wametakiwa kushirikiana  ili kuhakikisha wanamaliza kabisa changamoto hizo.

Hayo yamesemwa na  Afisa elimu msingi wilaya ya Pangani Bwana Mbwana Juma katika warsha ya uzinduzi wa ripoti hiyo ambapo mbali  na kuifurahia, amesema walimu wanapaswa kushirikiana na wadau ili kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni na kuongeza kiwango cha ufaulu.

“Taarifa hii kwa kweli imenifariji, imetupandisha hadhi, lakini changamoto iliyojitokeza moja wapo ni kwenye lishe, ingawa tunapata asilimia 17 kati ya 24 kitaifa, lakini bado inatubidi kuongeza juhudi, upande wa mahudhuria kwanini isiwe 100%, lakini kwa sasa 84% ya walimu ndio wanaohudhuria shuleni, basi isipofika 100 basi ifike hata 90%” alisema Bwana Juma



Nao wadau waliohudhuria katika warsha hiyo wameelezea kuguswa na ripoti hiyo huku wakitoa maoni yao katika kuboresha sekta ya elimu wilaya ya Pangani ikiwemo nidhamu na kuitumia Pangani FM kama chombo cha kukuza elimu.

“Nasisitiza kitu kimoja, nidhamu, kwa sababu hata ukisoma ukiwa Profesa kama huna nidhamu kwenye maisha yako utapata shida sana, sisi mpaka tumefika hapa, hatukua na alimu ya juu zaidi lakini tunaheshimu walimu wetu mpaka leo” Alisema mdau huyo.

“Nimeona hii nafasi niseme ili niitendee haki Pangani FM, hii redio imeifanya Pangani ifahamike kila sehemu ya nchi, inajulikana na sasa tuisaidie na kuitumia hii Pangani FM. Mfano kile kipindi cha watoto siku ya Jumamosi, wakae walimu ngazi ya Kata au Kiwilaya waandae maswali yatakayowasaidia hawa wanafunzi” alisema mdau mwengine.


Kwa upande wake Mratibu wa utafiti huo kutoka AFRIWAG Bwana Faraji Is-Haka amewataka wadau wote waliohudhuria katika uzinduzi wa ripoti hiyo kutoona matokea ya utafiti huo kama hukumu bali kuyatumia katika kujitathimini na kuboresha elimu wilayani Pangani.

“Hizi takwimu ni kwa ajili ya kujitathmini kama walivyotangulia kusema, tuone huu utafiti kama fursa kwetu sisi wadau na wananchi, kila mtu kwa nafasi yake  ndio maana ripoti imechukua maeneo menngi, mlo, waalimu, wanafunzi, ili kila mtu atekeleze wajibu wake kwa lengo la kufikia mafanikio” Alisema Bwana Faraji

Utafiti huo uliyofanyika mwaka 2015 umeonesha wilaya ya Pangani ikishika nafasi ya 63 kati ya 159 kitaifa huku kimkoa ikishika nafasi ya 4  ambapo pia suala la chakula shuleni ikiwa na 17% kati ya 24% kitaifa na mahudhurio ya wanafunzi na walimu ikipituka lengo la taifa.


No comments

Powered by Blogger.