JESHI LA POLISI (W) PANGANI LATHIBITISHA KUPATIKANA KWA MAITI NYENGINE YA WAVUVI WALIOZAMA BAHARINI



Siku moja baada ya jeshi la polisi wilayani Pangani kutangaza kupotea kwa watu wanne kwenye bahari hindi baada ya Boti ya uvuvi iliyokuwa na jumla ya watu 17 kuzama, ambapo kwenye taarifa ya awali ilieleza kuwa mtu mmoja alifariki, 12 kuokolewa, leo tena mtu mwengine amepatikana amefariki dunia ikiwa ni miongoni mwa wale wanne.

Kijana aliyepatikana ametambulika kwa jina la MOHAMED YUSUPH anaekadiriwa kuwa na umri wa miaka 29, ambapo mwili wake umepatikana  ukiwa unaelea juu ya maji katika maeneo ya Kokoni nje kidogo ya mji wa Pangani.

Akithibitisha kupatikana kwa mwili huo Kaimu Kamanda wa Polisi ambae ni mkuu wa kituo cha Polisi wilayani Pangani ASP MAYASA OMARY, amesema kuwa kutokana na tukio la Boti kuzama hapo jana  mapema leo hii wamefanikiwa kupata mwili mmoja ambao unakamilisha idadi ya watu wawili waliofariki dunia  ambapo mpaka sasa watu watatu bado hawajapatikana.

“Mwili umehifadhiwa katika hospitali ya wilaya hapa Pangani kwa ajili ya kuwasubiri ndugu wa marehemu, waje na kufanya taratibu za mazishi.” Alisema Mayasa

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa hospital ya wilaya ya Pangani KOMBO MUHINA, mbali na kukiri kupokea majeruhi 12 hapo jana, lakini pia leo amekiri kupokea mwili wa kijana Mohammed Yusufu ili kusubiri ndugu zake.

Hadi sasa inaelezwa kuwa watu watatu hawajapatikana mara baada ya chombo walichokuwa wakikitumia katika shughuli za uvuvi kupata dhoruba katika mkondo wa bahari ya hindi wilayani Pangani hapo jana.

No comments

Powered by Blogger.