WANANCHI WA KATA YA BWENI WILAYANI PANGANI WAMLALAMIKIA MTENDAJI WAO



Wananchi wa Kata ya Bweni wilayani Pangani wamelalamikia utendaji kazi wa Afisa mtendaji wa Kata hiyo kutokana na walichokiita kutofuata utaratibu na maadili ya utumishi wake.

Wakizungumza wakati wa Mkutano mkuu wa dharura ambao umefanyika mbele ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo katika kijiji cha Bweni, wananchi hao wamesema mtendaji huyo amekuwa akifanya mambo mbalimbali yasiyofaa ikiwemo kutoza pesa za barua, kutoa siri za serikali pamoja na kupoteza baadhi ya nyaraka za serikali, huku wakimuomba mkurugenzi huyo kumuondoa katika kata hiyo.

Awali katika mkutano huo Diwani wa Kata ya Bweni Bwana Kassim Saidi Omari ameelezea kusikitishwa na kitendo cha mwananchi mmoja kuteka eneo la zahanati na shule ya msingi Kikokwe, suala ambalo halijapatiwa ufumbuzi kutokana na kukosa ushirikiano na mtendaji huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Pangani Ndugu Sabas Damiani Chambasi, amesema masuala yote atakwenda kuyafanyia kazi kulingana na taratibu na sheria za kiutumishi, huku akiwaagiza baadhi ya viongozi wa kata na kijiji hicho kuhakikisha wataalamu wanaofanya kazi katika kata yao wanawajibika ipasavyo ili kuleta Maendeleo.

Hayo yamejiri katika Mkutano maalumu wa kujadili mgogoro wa uvamizi wa eneo la shule ya msingi na zahanati ya kikokwe kijiji cha Bweni, huku kikihudhuriwa na Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Pangani.

No comments

Powered by Blogger.