HALMASHAURI YA WILAYA YA PANGANI IMETAKIWA KUWEKA KIPAUMBELE KATIKA UCHUMI WA VIWANDA.



Halmashauri ya wilaya ya Pangani imetakiwa kuweka kipaumbele katika uchumi wa viwanda na kutumia rasilimali zilizopo ikiwemo bahari  ili kuongeza mapato kwa ajili ya kuleta maendeleo ya halmashauri ya wilaya hiyo.

Akizungumza  wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Pangani waliokusanyika katika uwanja wa ofisi ya kata ya Pangani Magharibi Kiongozi wa Mbio za mwenge wa Uhuru  kitaifa Bwana AMUR HAMAD AMUR  amesema hakuridhishwa na kiwango cha mapato kilichokusanywa na halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17 akisema inawezekana kuwa ni halmashauri ya kwanza kukusanya kiwango kidogo cha mapato.

Hata hivyo kiongozi huyo wa mbio za mwenge amewapongeza Viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Pangani kwa ushiriki  wao wa kuwezesha kuanzishwa kwa vikundi vya ujasiriamali vya vijana na wakina mama ambavyo vilizinduliwa na mbio za mwenge wa uhuru kitaifa 
 huku akisema  ni kitu cha pekee kuona uwepo wa vikundi vinavyofanya kazi nzuri katika wilaya ya Pangani tofauti na maeneo mengine aliyopita hivyo kuitaka halmashauri hiyo kuviongezea mikopo vikundi hivyo ili kukuza mitaji yao na kunyanyua uchumi  wao na halmashauri.

Kwa upande mwengine Kiongozi huyo amesikitishwa na kitendo cha uongozi wa  Halmashauri ya wilaya ya Pangani kutoviunga mkono vikundi  vinavyozalisha bidhaa mbalimbali  kwa kutonunua bidhaa za vikundi hivyo  ikiwemo kikundi cha AMANI VICOBA kinachojihusisha na uzalishaji wa Batiki katika mji wa Pangani.
Pamoja na hayo Bwana Amur amezindua miradi mitano ya kimaendeleo , mmoja kuweka jiwe la msingi na mmoja kufunguliwa yote ikiwa na thamani ya shilingi za kitanzania zaidi ya bilioni 2.


Mbio hizo za mwenge wa uhuru kwa wilaya ya Pangani zilipokelewa tarehe 29 mwezi wa 9 Mwaka 2017 katika kijiji cha Mkalamo ukitokea wilaya ya handeni na kukabidhiwa kwa wilaya ya Muheza katika kijiji cha mkuzi huku ujumbe wa mwenge wa uhuru kwa mwaka huu ni SHIRIKI KUKUZA UCHUMI WA VIWANDA KWA MAENDELEO YA NCHI YETU.
 

 




No comments

Powered by Blogger.