NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI JUMAA HAMIDU AWESO AFANYA ZIARA PANGANI
Naibu waziri wa maji na Umwagiliaji ambaye pia ni
Mbunge wa Jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso leo ameanza ziara
katika jimbo lake kwa kukutana na Wazee na viongozi wa dini katika jimbo la
Pangani kwa ajili ya kutoa shukurani zake pamoja na kujua changamoto
zinazowakabili wazee hao.
Akizungumza wakati
alipokutana na Wazee hao katika Ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya
Pangani Mheshimiwa Naibu waziri amewaomba wazee hao kuwekeza kielimu kwa watoto
wao huku akimtaka Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo kuhakikisha wazee wanapata huduma za Afya bure.
Kwa upande wao wazee waliohudhuria katika kikao
hicho mbali na kumpongeza wamemuomba Naibu waziri huyo kutafuta mbinu
mbalimbali kwa ajili ya kutumia maeneo
yenye fursa ya umwagiliaji pamoja na kutatua kero ya wafugaji kuingiza
mifugo yao katika mashamba ya wakulima ili kuisaidia sekta ya kilimo kupiga
hatua katika wilaya ya Pangani.
Pia Mkuu wa wilaya ya Pangani Bi Zainabu Abdallah
Issa amemuomba Naibu waziri huyo kutumia fursa na ushawishi alionao sasa kwa
ajili ya kufanikisha maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo upatikanaji wa maji
safi na barabara ya lami.
Hata hivyo Naibu waziri huyo amesema ameyapokea
maombi hayo huku akisema tayari katika kipindi alichokuwa madarakani kama
mbunge kuna mambo mbalimbali ya kimaendeleo anayahangaikia ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa meli ya kutoka Pangani Mpaka Zanzibar.
Hayo yanakuja ikiwa ni siku chache baada ya
kuteuliwa na Mheshimiwa Rais kuwa Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji ambapo
wazee mbalimbali katika jimbo la Pangani wamezungumzia kufurahishwa na hatua
hiyo aliyoifikia.
No comments