ZAIDI YA KILO SITINI ZA SAMAKI WALIOVULIWA KWA UVUVI HARAMU ZAKAMATWA WILAYANI PAGANI
Zaidi ya kilo sitini (60) za Samaki waliovuliwa kwa
uvuvi haramu wa milipuko ya mabomu zimekamatwa wilayani Pangani Mkoani Tanga,
kufuatia doria zinazoendelea za kudhibiti shughuli za uvuvi huo Wilayani humo.
Akizungumza na Pangani fm Afisa doria Uvuvi Wilayani
Pangani Bwana Jorwam Rebo, amesema kuwa jana wakati akiwa kwenye doria na timu
yake wakishirikiana na kamati ya BMU katika kijiji cha Bweni wilayani humo, wamefanikiwa
kukamata mzigo ambao baada ya kuukagua wamejiridhisha kwamba ni samaki waliovuliwa
kwa milipuko ya mabomu.
“Na mpaka sasa muhusika tumemfikisha katika vyombo
vya dola na taratibu za kisheria zinaendelea” amesema.
Aidha Bwana Jorwam amesema kuwa pamoja na jitihada
ambazo wamekuwa wakizifanya katika kudhibiti uvuvi haramu kwa kushirikiana na
vyombo vya dola, kwa kiasi kumekuwa na woga kwa watu kutumia uvuvi haramu
ijapokuwa wengi wao wamekuwa wakitekeleza shughuli hizo kwa kujificha.
“Wilaya zetu za jirani ndo zinachangia kwa kiasi
kikubwa shughuli za uvuvi haramu hapa kwetu, kwani hata ukiangalia samaki
tuliowakamata, hawa ni wavuvi amabo wametoka kijiji cha mwarongo ambacho kipo
halmashauri ya jiji la TANGA, na kwasababu tulikuwa tunawafatilia wametukimbia na
kurejea kwao”amesema Bwana Jorwam.
Ameongeza kuwa katika kudhihirisha wao hawako pamoja
na watu wa uvuvi haramu na wanaofanya biashara hizo, wataendelea kufanyakazi kila
siku hasa katika maeneo yaliyokithiri shughuli za uvuvi haramu Ushongo, Sange, Kipumbwi
na Mkwaja.
“Kikazi tumejidhatiti sana, unavyoona tunafanya
doria za kushtukiza, tunapata taarifa, tunaenda bila watu kujua na sisi
tunajiridhisha tunakamata. Waendelee kutuamini na tuendelee kupeana taarifa
tutaifanya kazi” amesema Jorwam.
Shughuli za uvuvi haramu Wilayani Pangani hufanyika
kwa ushirikiano kati ya watu kutoka nje ya Pangani na baadhi ndani ya Wilaya,
ambapo mpaka sasa jumla ya wavuvi 1570 Wilayani humo wanatambulika kisheria,
ukiachilia mbali wengineo wanaoendelea kufanya shughuli hizo kwa njia zisizo
rasmi.
No comments