WAMILIKI WA MASHINE ZA KUSAGA NA KUKOBOA WILAYANI PANGANI WATAKIWA KUFUATA UTARATIBU
Baadhi ya wakazi wilayani Pangani wamewalalamikia
wamiliki wa mashine za kusaga na kukoboa Mahindi kwa kutojali muda wa
kufanyakazi hali ambayo inaleta kero kutokana na kelele zinazotokana na mashine
hizo hasa nyakati za usiku.
Wakizungumza na Pangani Fm baadhi ya majirani walio
karibu na mashine hizo wameeleza kuwa mashine hizo zilizopo maeneo ya makazi
yao, hufanya kazi hadi saa nne au saa sita usiku, hali ambayo inawafanya
washindwe kupumzika.
Mbali na kelele, pia wananchi hao wameongeza kuwa, uwepo
wa mashine hizo katikati ya makazi ya watu umekuwa ni kero kutokana na nguvu za
mashine hizo zinazotoa mtikisiko unaosababisha nyumba zao kuota nyufa.
Kwa upande wake Afisa Mazingira wa wilaya Pangani Bwana
DAUDI MLAHAGWA amesema kuwa kwa mujibu wa sheria ya viwanda vidogo kama mashine
ya kusagia Mahindi pia ipo kwenye daraja la kiwanda kidogo huku akibainisha
madhara wanayo tambulika kisheria ni kuwa ni pamoja na vumbi la unga, Moshi na mngurumo
wa mashine.
Aidha Bwana MLAHAGWA amesema “Viwanda ambavyo vipo
kwenye makazi ya watu ni hivi vidogo huwa tunasema angalu saa kumi na mbili
jioni viwe vimfungwa kwa sababu jioni ni muda wa kupumzika, sasa ikiwa familia
inataka kupumzika halafu bado kiwanda kinafanya kazi itakua ni usumbufu”
MLAHAGWA amewataka wamiliki wa mashine za kusaga na
kukoboa zilizopo wilayani Pangani kuzingatia sheria na kufunga mapema mashine
hizo ili kuondoa usumbufu kwa wananchi, vinginevyo sheria itachukua mkondo
wake.
No comments