MHESHIMIWA AWESSO KUANZA ZIARA YA KIKAZI WILAYANI PANGANI KESHO
Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini ambaye
pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani Mheshimiwa Jumaa Hamidu Aweso kesho
anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi ya jimboni kwake, kwa lengo la kusikiliza
kero za maji na kuzitatua.
Akizungumza na Pangani fm mapema jioni hii katibu
msaidizi wa Mbunge wa Jimbo la Pangani Ndugu Salumu Kanyama, amesema Naibu Waziri
huyo ambaye ataanza ziara yake Wilayani Pangani hapo kesho tarehe 27 hadi 29
mwezi huu, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maeneo atakayotembelea.
“Kwa hiyo ataanza kuzungumza na wazee wa Pangani
pale katika ukumbi wa halmashauri ya Pangani kuanzia saa nne kamili asubuhi,
halafu saa saba mchana atafanya kikao na wakuu wote wa idara ya halmashauri
pamoja na wataalamu wote, na kisha jioni atamalizia na mkutano wa hadhara
katika eneo la sokoni hapa Pangani Mjini”
alisema Kanyama.
Mbali na kuanza ziara hiyo kesho, lakini pia Naibu
Waziri huyo atakuwa na kazi maalumu mkoani Tanga na kisha ataendelea na ziara yake fupi Wilayani Pangani
siku ya Jumapili, pamoja na kwenda kutoa tamko la matumizi sahihi ya kiasi cha
shilingi za Kitanzania Milioni 500.8 ambacho kimeshaingizwa katika kijiji cha MTANGO
kata ya Ubangaa kwa ajili ya mradi wa Maji.
Katika hatua nyingine Bwana Kanyama ameongeza kuwa
kufuatia siku chache za ziara hiyo, amewatoa hofu wananchi wa Pangani kuwa
baada ya Naibu waziri wa Maji na Umwagiliaji Muheshimiwa AWESO kumaliza vikao
vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, atafanya ziara kubwa katika vijiji
vyote vilivyopo wilayani Pangani.
Ziara hii ni ahadi ambayo Naibu waziri wa maji na
umwagiliaji nchini ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Pangani Muheshimiwa Jumaa
Hamidu Aweso aliitoa kuwa ataifanya baada ya kumaliza ziara yake ya kikazi
mkoani SHINYANGA, ambapo ziara hii ataifanya kwa ajili ya kuzungumza na
wananchi wa jimbo lake, huku akiambatana na timu yake ya wizara ya maji ili
kuja kupanga mikakati ya pamoja katika kutatua changamoto ya maji hususani kwa
maeneo ambayo yana shida kubwa ya upatikanai wa huduma hiyo.
No comments