"MTU MMOJA AFARIKI DUNIA BAADA YA KUZAMA KWENYE MTO PANGANI"- JESHI LA POLISI (W) PANGANI



Mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Sechambo Hasani Sechambo mwenye umri wa miaka 60 amekufa maji katika kijiji cha Kigurusimba Wilayani Pangani, baada ya Mtumbwi aliokuwa amepanda kuzama.

Akithibitisha tukio hilo kaimu Mkuu wa Polisi Wilayani Pangani ambaye ni mkuu wa kituo cha Polisi Pangani Bi Mayasa Omary Sefu, amesema mtu huyo ambaye ni mkulima amekufa maji kufuatia mtumbwi wao kuzama baada ya kukumbwa na dhoruba walipokuwa wakivuka Mto Pangani kutoka kijiji cha Kigurusimba kuelekea kijiji cha Mseko.

Aidha Bi Mayasa amesema Marehemu huyo ni mwenyeji wa Bumbuli wilayani Lushoto, ambapo baada ya kufanyiwa uchunguzi tayari mwili wake umekabidhiwa kwa ndugu tayari kwa ajili ya mazishi.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Kituo cha Polisi Pangani Bi Mayasa Omary ametoa wito kwa watumiaji wa Mto na Bahari Wilayani humo, kuendelea kuchukua tahadhari hasa katika kipindi hiki cha upepo mkali ili kuepukana na vifo.

No comments

Powered by Blogger.