RIPOTI YA AFRIWAG YAZINDULIWA RASMI LEO WILAYANI PANGANI
Kufuatia ripoti ya utafiti
na tathmini iliyoandaliwa na taasisi ya AFRIWAG na Twaweza kuonyesha uwepo wa
changamoto ya upatikanaji wa chakula shuleni huku kiwango cha mahudhurio ya
wanafunzi na walimu kikionekana kupita makadirio ya taifa, walimu na wadau wa
elimu Wilaya ya Pangani wametakiwa kushirikiana
ili kuhakikisha wanamaliza kabisa changamoto hizo.
Hayo yamesemwa na Afisa elimu msingi wilaya ya Pangani Bwana
Mbwana Juma katika warsha ya uzinduzi wa ripoti hiyo ambapo mbali na kuifurahia, amesema walimu wanapaswa
kushirikiana na wadau ili kusaidia upatikanaji wa chakula shuleni na kuongeza
kiwango cha ufaulu.
“Taarifa hii kwa kweli
imenifariji, imetupandisha hadhi, lakini changamoto iliyojitokeza moja wapo ni
kwenye lishe, ingawa tunapata asilimia 17 kati ya 24 kitaifa, lakini bado
inatubidi kuongeza juhudi, upande wa mahudhuria kwanini isiwe 100%, lakini kwa
sasa 84% ya walimu ndio wanaohudhuria shuleni, basi isipofika 100 basi ifike
hata 90%” alisema Bwana Juma
Nao wadau waliohudhuria
katika warsha hiyo wameelezea kuguswa na ripoti hiyo huku wakitoa maoni yao
katika kuboresha sekta ya elimu wilaya ya Pangani ikiwemo nidhamu na kuitumia
Pangani FM kama chombo cha kukuza elimu.
“Nasisitiza kitu
kimoja, nidhamu, kwa sababu hata ukisoma ukiwa Profesa kama huna nidhamu kwenye
maisha yako utapata shida sana, sisi mpaka tumefika hapa, hatukua na alimu ya
juu zaidi lakini tunaheshimu walimu wetu mpaka leo” Alisema mdau huyo.
“Nimeona hii nafasi
niseme ili niitendee haki Pangani FM, hii redio imeifanya Pangani ifahamike
kila sehemu ya nchi, inajulikana na sasa tuisaidie na kuitumia hii Pangani FM.
Mfano kile kipindi cha watoto siku ya Jumamosi, wakae walimu ngazi ya Kata au
Kiwilaya waandae maswali yatakayowasaidia hawa wanafunzi” alisema mdau
mwengine.
Kwa upande wake Mratibu
wa utafiti huo kutoka AFRIWAG Bwana Faraji Is-Haka amewataka wadau wote
waliohudhuria katika uzinduzi wa ripoti hiyo kutoona matokea ya utafiti huo
kama hukumu bali kuyatumia katika kujitathimini na kuboresha elimu wilayani Pangani.
“Hizi takwimu ni kwa
ajili ya kujitathmini kama walivyotangulia kusema, tuone huu utafiti kama fursa
kwetu sisi wadau na wananchi, kila mtu kwa nafasi yake ndio maana ripoti imechukua maeneo menngi,
mlo, waalimu, wanafunzi, ili kila mtu atekeleze wajibu wake kwa lengo la
kufikia mafanikio” Alisema Bwana Faraji
Utafiti huo
uliyofanyika mwaka 2015 umeonesha wilaya ya Pangani ikishika nafasi ya 63 kati
ya 159 kitaifa huku kimkoa ikishika nafasi ya 4
ambapo pia suala la chakula shuleni ikiwa na 17% kati ya 24% kitaifa na
mahudhurio ya wanafunzi na walimu ikipituka lengo la taifa.
No comments