WAKULIMA PANGANI WAIPONGEZA IDARA YA KILIMO KWA KUWAELIMISHA KUHUSU ZAO LA KOROSHO.
Idara ya kilimo wilayani Pangani imepongezwa kwa jitihada zake za kuelimisha wakulima katika zao la korosho jambo
lililopeleka wakulima hao kutumia njia mbalimbali za kitaalamu ikiwemo kupulizia
dawa na kulimia mikorosho yao kwa wakati.
Akizungumza na Pangani FM Mkulima mmoja wa zao hilo
kutokea kijiji cha Sange aliyejitambulisha kwa jina la ALBANO PETER MWALIDO amesema
kutokana na hali hiyo imewawezesha wakulima kupata mavuno mengi katika msimu
huu.
‘’Kwenye
elimu ya mikorosho kwa kweli serikali imejitahidi na halmashauri pia
imejitahidi, imehamasisha na kuelekeza wakulima hasa kata ya mkwaja wakulima
wengi wanaendana na wakati watu wengi walijitahidi kusafisha mashamba na
kupulizia dawa jambo ambalo limepelekea wakulima wengi kuvuna korosho’’amesema Albano.
Mbali na mafanikio hayo Bwana Albano amesema bado
wanaathiriwa na kuchelewa kwa msimu mpya wa mnada wa korosho, hali inayopelekea baadhi ya wakulima kuuza
mazao yao kwa wafanyabiashara wa maduka kwa bei ndogo.
‘’wakulima wengi wana korosho ndani
wengine wana gunia tatu hadi nne lakini changamoto kubwa hawajui watamuuzia
nani, na zitauzwa lini, sasa kilichokuwepo mkulima huyu analanguliwa.’’ Amesema Albano.
Kwa upande wake Afisa kilimo wa wilaya ya Pangani
Bwana RAMADHANI ZUBERI amesema wakulima wanapaswa kupeleka mazao yao kwenye
chama cha ushirika katika kijiji cha Mikocheni, ili kuwezesha kupata idadi
kamili ya mazao yote ndipo waitishe mnada.
‘’Wakulima
wote kila mmoja korosho zake apelike kwenye chama cha ushirika pale wakazipime
zipo kiasi gani ili baadae tutakapo zikusanya tutatangaza kwenye bodi na ili
kutafuta mnunuaji na huo ndo utaratibu ulio pangwa kuwa korosho haziuzwi kwa
kilo moja moja’’ amesema Zuberi.
Zao la korosho ni miongoni mwa mazao ya biashara
nchini Tanzania ambalo limeonekana kuwanufaisha wakulima wa zao hilo kutokana
na kutumika mfumo wa mnada hususani katika mikoa ya lindi na mtwara, huku
katika wilaya ya Pangani idara ya kilimo ikiendeleza jitihada zake katika
kuinua thamani ya zao hilo.
No comments