UPATIKANAJI WA MAJI PANGANI MJINI WAIMARIKA BAADA YA UKARABATI WA MIUNDOMBINU
Zoezi la ukarabati wa miundombinu ya Maji wilayani
Pangani hususani Pangani Mjini hatimae umekamilika, huku ikikadiriwa eneo lenye
urefu wa mita 3350 likipata maji kwa uhakika.
Akizungumza na Pangani FM meneja wa Mamlaka ya Maji
na Usafi wa Mazingira Pangani Mjini Bwana Adamu Waziri Sadiki, pamoja na
kuthibitisha ukamilifu wa zoezi hilo amesema kuwa kwa wateja ambao wamepitiwa
na ukarabati huo na bado hawapati huduma ya maji, wafike kwenye ofisi zao
zilizopo katika jengo lilokuwa ofisi ya mkuu wa wilaya zamani ili kuwasilisha
matatizo yaliyopo
‘’lile zoezi letu la kuifanyia ukarabati
miundombinu ya maji hasa maeneo ya pangani mjini limekamilika na limetumia
takribani urefu wa mita 3350, kama kuna mwananchi hapati maji afike ofisini
kwetu’’ amesema meneja wa maji.
Pia Bwana Adamu ameongeza kuwa wadaiwa sugu
hawatapata huduma ya maji hadi watakapolipa madeni yao, na kwamba ili huduma
hiyo ikidhi mahitaji ni lazima wateja kulipa kwa wakati.
‘’pia kuna
watu ambao ni wateja wetu ni wadaiwa sugu, kwa hiyo watu kama hawa
hatukuwaunganishia maji, tunaomba mje mlipe na ukiona bomba limepita na huja
unganishiwa ujuwe ni mmoja wa wadaiwa sugu mlipe ili tuwaunganishie’’ ameongeza
tena.
Ukarabati wa miundombinu mipya ya maji Pangani Mjini
umehusisha ufukuaji wa mabomba chakavu na kufukia mapya, na hii ni katika
mpango wa kuhakikisha huduma ya maji safi na salama unawafikia wananchi wote
kwa urahisi.
No comments