MHESHIMIWA AWESSO AISHUKIA MAMLAKA YA MAJI PANGANI MJINI, AIPA MASAA 24 MAJI YAPATIKANE
Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji nchini Mheshimiwa Jumaa
Hamidu Awesso ameitaka Mamlaka ya Maji Pangani Mjini (PAWASA), kuhakikisha hadi
kufikia kesho tarehe 05/12/2017, hali ya upatikanaji wa maji inatengemaa katika eneo la Pangani
Mjini kabla ya hatua za kinidhamu kuchukuliwa.
Akizungumza na Pangani Fm kwa njia ya simu mapema leo, Naibu
Waziri huyo ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Pangani amesema kuwa, amepata
taarifa kuwa hali ya upatikanaji wa Maji Pangani Mjini sio wa kuridhisha, hivyo
kuitaka Mamlaka husika kuchukua hatua haraka.
“Nimepata taarifa kuwa hapo Pangani Mjini leo ni siku ya
tatu au ya nne maji hakuna kabisa, na hakuna taarifa yoyote, sasa nataka
niwaombe mamlaka ya maji Pangani Mjini, wahakikishe maji yanapatikana kesho,
ili wananchi wapate maji, kama kuna kikwazo chochote watoe taarfa mapema kabla
hatujaanza kuchua hatua kwa watendaji wakuu” alisema Mheshimiwa Awesso.
Hivi karibuni Mamlaka ya Maji Pangani Mjini kupitia kaimu
meneja wake Bwana John Kisiwa, iliwaomba radhi wateja wake kufuatia kuharibika
kwa mashine ya kupandishia maji iliyopo eneo la Boza, Mheshimiwa Naibu Waziri akatoa
wito kwa Mamlaka hiyo kufuatia kuharibika kwa mashine hiyo
“Mashine hata kama imeharibika inatakiwa kurekebishwa kwa
wakati ili wananchi wapate maji kwa maana wao hawafahamu, kwa hiyo ninachotaka
mamlaka itimize wajibu wao ili kutatua tatizo hilo, wafanye kazi usiku na
mchana ikiwezekana, lakini waone umuhimu wao kwa jamii” alisema Mheshimiwa
Naibu Waziri.
Katika hatua nyengine Mheshimiwa Jumaa Awesso ameweka bayana
adhma ya serikali katika kuboresha huduma ya upatikanaji maji katika maeneo ya
Mbugani, Langoni pamoja na eneo la Masaika, huku akiwataka wataalamu kutoka
Halmashauri ya Pangani kuwashirikisha wananchi wa maeneo hayo ili kujua vyavyo
sahihi vya upatikanaji maji.
“Sasa hivi visima tutakavyochimba ni eneo la Mbugani, Langoni
lakini wananchi wetu wa Masaika wamekuwa na tatizo kubwa la maji, wataalamu
walichimba kwa mara ya kwanza lakini hawakufanikiwa, lakini sasa niwaombe
wataalamu wa Halmshauri wawashirikishe awamu hii wakienda kuchimba basi
wawashirikishe wananchi wa Masaika katika kutambua vyanzo sahihi vya maji”
Alisema Mheshimiwa Jumaa Awesso.
Mheshimiwa Jumaa Awesso ambaye anatarajiwa kufanya ziara ya
kikazi mkoani Singida hivi karibuni, amewaomba wananchi wilayani humo kutunza
vyanzo vya maji kwa lengo la kutokukwamisha huduma hiyo muhimu kwa maisha ya
binadamu.
No comments