SHINDANO LA VMAC 2017 WILAYANI PANGANI LAZINDULIWA RASMI

Hatimae shindano la kutafuta kamati bora za kudhibiti ukimwi, Jinsia na Uongozi, Kijana bora wa mfano wa kuigwa pamoja na Mwanamke bora kwa mwaka 2017/2018 limezinduliwa rasmi leo huku likiwa na muonekano wa kipekee.

Akizungumza na Pangani Fm leo, mratibu wa masuala ya jinsia na uongozi kutokea shirika la Uzikwasa Bi Salvata Kalanga amesema kuwa, tayari mchakato huo umefikia hatua za mwisho na muda sio mrefu watatangaza kilele cha shindano hilo.

"Ni kwamba kila kitu kipo tayari, na leo tunazindua rasmi shindano hili ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu, hivyo kila kamati ikae mkao wa ushindani kwa kuwa mwaka huu kuna mabadiliko makubwa" alisema Bi Salvata.

Mbali na kuzindua shindano hilo kupitia kipindi cha Asubuhi Ya Leo kinachorushwa na Pangani Fm, Bi Salvata alitumia nafasi hiyo kuzitaja kamati 17 bora kati ya kamati 33 zitakazoingia kwenye mchujo wa awali.

Kamati hizo zilizoingia kwenye nafasi ya 17 bora ni pamoja na kamati ya kudhibiti Ukmiwi, Jinsia na Uongozi ya kijiji cha Mwera, Kijiji cha Mzambarauni, Kijiji cha Mseko, Kijiji cha Mikinguni, Kijiji cha Mtonga, Kijiji cha Kimang'a, Kijiji cha Mbulizaga, Kijiji cha Mwembeni, Kijiji cha Tungamaa, Kijiji cha Mikocheni na Kijiji cha Sange.

Vijiji vyengine ni pamoja na Mkwajuni, Msaraza, Kijiji cha Pangani Mashariki, Kijiji cha Kwa Kibuyu na Kijiji cha Bweni ambavyo vyote vimeinesha utekelezaji mzuri wa vigezo vya shindano hilo.

Bi Salvata kalanga pia amezitaka kamati zote zilizoingia kwenye hatua ya 17 bora kufika kwenye ofisi za Uzikwasa tarehe 12/12/2017 majira ya saa mbili asubuhi kwa ajili ya mchujo wa mwisho. Shindano hilo limebeba kauli mbiu isemayo "LISILOWEZEKANA, LINAWEZEKANA"

Shindano la kutafuta kamati bora za kudhibiti Ukimwi, Jinsia na Uongozi huratibiwa na shirika la Uzikwasa lenye maskani yake wilayani Pangani ambapo kwa mwaka jana mshindi wa shindano hili kilikuwa ni kijiji cha Mseko.

No comments

Powered by Blogger.